Back to top

Wafugaji wachomewa nyumba na mazao katika maeneo wanayodaiwa kuvamia.

12 September 2018
Share


Nyumba kadhaa za wafugaji katika Kata ya Kitanga Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma zimechomwa moto pamoja na mazao, kufuatia mgogoro kati ya wakulima na wafugaji na wengine wakijeruhiwa baada ya serikali kuagiza wafugaji waondoke katika eneo la msitu katika Kata hiyo wanayoyakalia kinyume cha sheria.

Wafugaji jamii ya Wasukuma wakizungumza katika maeneo mbalimbali ya Kata hiyo, wamesema tangu kutolewa kwa amri ya kuwataka waondoke, wamekuwa wakivamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa wakazi wa Kata hiyo na kuporwa mazao na mifugo huku  nyumba zao mazao yaliyohoifadhiwa vikiteketezwa kwa moto.

Hali hiyo imewafanya wakimbie hovyo na wameiomba serikali kuingilia kati mgogoro huo ambao mwezi uliopita ulisababisha vifo vya watu wanne.

Mwenyekiti wa Wafugaji Kanda ya Magharibi, Bwana KUSUNDWA WAMALWA amesema machafuko yanayoendelea yanatokana na serikali kuacha oparesheni ya kuwaondoa wafugaji kufanywa na wanakijiji hali ambayo imesababisha madhara na kuendelea kwa machafuko.

Akizungumza suala hilo hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali SIMON ANANGE amesema ni jukumu la halmashauri kupanga maeneo ya kuwapeleka wafugaji hao, lakini mpango wa kuwaondoa kwenye maeneo wanayoishi kinyume cha sheria uko palepale .