Back to top

Wafugaji walalamikia maeneo ya malisho kuvamiwa na wakulima Handeni

17 February 2019
Share

Wananchi wa kijiji cha Msomela kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga ambacho kimetengwa kwaajili ya malisho wamelalamikia kitendo cha baadhi ya wakulima kuvamia maeneo yao na kuyageuza kuwa ya kilimo  hali inayosababisha mapigano ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima .

Akisoma taarifa ya kijiji hicho mbele ya kamati ya usalama ya wilaya mtendaji wa kijiji hiki cha Msomela wakati wa kukabidhiwa hati ya kijiji hicho ambacho kilianzishwa kwa dhumuni la wafugaji amedai kuwa kwa sasa kijiji hicho sio cha wafugaji tena ila kimekuwa cha wakulima na hali hiyo imekuwa ikisababisha migogoro ya mara kwa mara.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama wilayani hapa ambae pia ndie mkuu wa wilaya ya Handeni Godwin Gondwe baada ya kukabidhi hati hiyo kwa viongozi wa kijiji hicho amesema kuwa migogoro mingi ya wakulima na wafugaji husababishwa na baadhi ya viongozi wa vijiji kwa kuuza baadhi ya maeneo yaliotengwa kwaajili ya matumizi ya kilimo au ya mifugo na hivyo hatarajii kusikia hali hiyo tena baada ya kukabidhi hati hiyo ya kijiji.

Hata hivyo akawaagiza wananchi kutoa taarifa pale wanaposikia yupo kiongozi kwenye kijiji chao anataka kuuza eneo na serikali itawachukulia hatua viongozi wa namna hiyo maana hakuna alie juu ya sheria.