Back to top

Wakazi wa Bariadi watakiwa kuchagua viongozi wenye mtazamo mmoja.

17 September 2020
Share

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Ta ifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe.Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Bariadi wachague viongozi wenye mtazamo mmoja ili kuleta maendeleo ya haraka.

Ametoa wito huo leo alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Nkololo, Wilaya ya Bariadi, Mkoani Simiyu kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nkololo'A'.

Alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea Urais wa Chama hicho Dk.John Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi, Injinia Kundo Mathew, mgombea udiwani wa Kata ya Nkololo, Nyamwela Singida na wagombea udiwani wa kata zote za Wilaya ya Bariadi waliokuwepo kwenye mkutano huo.

Akizungumza na wakazi hao, Mhe.Majaliwa amesema Chama cha Mapinduzi kimetekeleza ahadi yake ya kuboresha miradi ya maji kwa kutoa  Shilingi Bilioni 3.2 zilizotumika kwenye vijiji vya Nkololo, Igaganulwa, Mwamlapa, Kasoli, Sengerema, Sanungu, Mahina, Nyangokolwa Masewa, Nyakabindi na Bupandagila.

Akielezea yaliyofanyika chini ya Ilani iliyopita ya Chama cha Mapinduzi Mhe.Majaliwa amesema Shilingi bilioni 1 na milioni 800  zimetolewa kwa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje ambalo sasa linatumika na majengo ya utawala, famasi, kufulia, maabara, mionzi, wodi ya wazazi ambayo yapo katika hatua ya ukamilishaji ya kuweka milango.