Back to top

Wakulima wadai fidia Bodi ya Pamba baada ya kupata hasara.

10 June 2018
Share

Wakulima waliolima  zao la pamba msimu huu wa kilimo katika kata nne za halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara wamesema hawaoni sababu ya kuacha kuidai fidia bodi ya taifa ya pamba sanjari na kituo cha utafiti wa mbegu ya pamba cha Ukiriguru kanda ya Mashariki kutokana na kuwahamasisha kutumia mbegu mpya ya pamba iliyoshindwa kuonyesha matokeo chanya ya uzalishaji na kuwasababishia hasara ya mamilioni ya fedha.

Diwani wa kata ya Mwadabw Gerald Chembe  amewasilisha malalamiko hayo kwenye kikao cha Mkuu wa mkoa Manyara Bw Alexander Mnyeti cha kujitambulisha kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya Babati na kusikiliza kero,huku baadhi ya wakulima  wakizungumza na itv wamesema mbegu hiyo imeathiri zaidi ya ekari 2,800 zenye mavuno hafifu.

Nae Mkuu wa Idara ya kilimo Ushirika na Umwagiliaji (DAICO) wa Halmashauri ya wilaya ya Habati vijijini  Bi Jetrida Kyekaka katika kikao hicho cha Mkuu wa mkoa amekiri kuwepo kwa athari hiyo.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Manyara Bw Alexander Mnyeti licha ya kupokea malalamiko ya wakulima  kuwepo kwa baadhi ya makampuni ya mbegu za mahindi kusambaza mbegu dhaifu,ikiwemo bodi hiyo ya pamba kuwasambazia mbegu zenye matokeo hasi amewataka kukusanya ushahidi wa kuyachukulia hatua za kusheria.