Back to top

Wakurugenzi waliochota fedha za NIDA kifisadi wakamatwa.

21 August 2018
Share

Wakurugenzi wa makampuni matatu yanayodaiwa kuchota kifisadi zaidi ya shilingi bilioni 3.99 za mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA wamekamatwa na jeshi la polisi baada ya kushidwa kutii agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola la kurejesha fedha hizo za serikali ndani ya siku 14.

Makampuni hayo ni Gotham International LTD, ASTE Insurance Brokers LTD na Gwilotho Impex LTD ambayo yanahusika na masuala ya ushauri, uwakala wa forodha na bima ambayo kwa nyakati tofauti yaliiingia kandarasi ya kutoa huduma kwa wakala huo.

Akitoa amri ya kukamatwa kwa wakurugenzi hao na Mkurugenzi wa makosa ya jinai Waziri wa Mambo ya ndani Mhe. Kangi Lugola amesema wameshindwa kurejesha fedha hizo ndani ya muda walioomba na serikali haina haiwezi kuvumilia tena.

Waziri Lugola pia ameagiza kukamatwa kwa aliyekuwa mkurugenzi wa NIDA Dicson Maimu na wafanyakazi wote wa mamlaka hiyo ambao walihusika na hujuma na uchotwaji wa feha hizo mara moja.

Aidha makampuni mengine matatu yaliyotajwa kwenye sakata hilo ambayo ni Iris Corporation, Sykes Travel Agent na Copy Cat Tanzania LTD zamani ikifahamika kama BMTL wamefanikiwa zaidi ya kurejesha shilingi bilioni 575 kwa fedha taslimu na makubaliano maalum kati yao na serikali.

Sakata la uchotaji wa fedha hizo za nida liliibuliwa kwenye ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wahesabu za serikali CAG ya mwaka 2016 ripoti ambayo Mhe. Rais John Pombe Magufuli alimuagiza waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola kufuatilia urejeshwaji wa fedha hizo wakati alipomteua kuwa Waziri.