Back to top

Walimu kuendelea kulipwa mishahara.

03 May 2020
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Mei, 2020 amemuapisha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Chato Mkoani Geita.


Mhe. Rais Magufuli amerejea kauli yake ya kuwataka Watanzania kutokuwa na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchukua tahadhari kama zinavyoelekezwa na wataalamu.


Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Walimu ambao ni asilimia 49 ya wafanyakazi wote hapa nchini pamoja na wafanyakazi wengine kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na ugonjwa wa Corona, Serikali imejipanga kuhakikisha wanalipwa mishahara yao kama kawaida na ametoa wito kwa taasisi za kifedha za kimataifa zilizoonesha nia ya kusaidia uchumi wa nchi zinazoendelea, kusamehe mikopo badala ya kutaka kuzikopesha mikopo mipya.


Mhe. Rais Magufuli amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe (aliyeteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni) kwa kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa vifaa vya uchunguzi wa ugonjwa wa Corona na ameagiza maabara kuu ya Taifa inayofanya uchunguzi wa ugonjwa huo ichunguzwe vizuri ili kujiridhisha juu ya usahihi wa majibu ya sampuli zinazopelekwa kuchunguzwa.


Amewataka Watanzania wote hasa wanasiasa pamoja vyombo vya habari kuacha kueneza taarifa zinazowajaza watu hofu ama kutumia ugonjwa huu kwa manufaa ya kisiasa na badala yake waungane kutoa elimu sahihi na kuhimizana kuchukua tahadhari za kutoambukizwa.

Ameelezea kushangazwa kwake na viongozi ambao wanazuia watu wanaofariki dunia kusafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao, na Viongozi wa Dini walioonesha kutetereka kiimani, hivyo ametoa wito kwa viongozi wote kusimama imara, kuonesha uongozi wa kweli na kuwapa matumaini wananchi badala ya kuwajaza hofu.