Back to top

Waliohusika mauji ya Sengondo Mvungi wahukumiwa kunyongwa hadi kufa.

18 September 2020
Share

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu kunyongwa hadi kufa watu watano, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt.Sengondo Mvungi miaka saba iliyopita.

Waliohukumiwa ni pamoja na Msigwa Matonyaz, Mianda Saluwa, Paulo Mdondono, Longishu Losingo na John Mayunga wakati Juma Kang'ungu akiachiliwa huru na mahakama hiyo baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake pasipo shaka.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Seif Kulita ambapo upande wa mashitaka uliwakilishwa na mawakili, Credo Rugaju, Llilian Lwetabura, Veronica Mtafya ambapo upande wa mashitaka katika kesi hiyo uliwasilisha mashahidi 16 na vielelezo 15.

Akitoa hukumu hiyo Jaji Kulita amesema ameridhika pasi na shaka na ushahidi wa upande wa mashitaka, hivyo anawahukumu washitakiwa wote kunyongwa hadi kufa isipokuwa mshitakiwa wa tano ambaye ni Juma Kang'ungu ambaye ushahidi wa mashitaka haumkumgusa.

Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na washitakiwa hao kufikishwa ni Novemba 22, 2013 .