Back to top

Wananchi Ihumwa wakubali kulipwa fidia kupisha ujenzi wa reli Kisasa

23 May 2018
Share

Hatimaye wananchi wa kata ya Ihumwa mkoani Dodoma wamekubali kulipwa fidia ili kupisha maeneo yao kwa ajili ya kuanza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendo kasi SGR kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma ambapo mkuu wa mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge amelitaka shirika la reli nchini TRL kukamilisha zoezi la uthamini wa ardhi na mali za wananchi hao ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na kamati ya ulinzi na usalama mkoani Dodoma baadhi ya wakazi wanaopitiwa na mradi huo wamesema wanakubali uwepo wa mradi wa reli ya kisasa ambapo wameiomba serikali kufanya tadhimini halisi ya fidia ili wananchi wapate haki zao.

Naye mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge amesema ni dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wanapata haki zao ambapo amewagiza udhamini kufanyika mapema huku akitoa onyo kwa watu wanaoshawishi wananchi kutokubali mradi huo.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa shirika la reli nchini TRL Bwana Masanja Kadogosa anawataka wakazi wa Ihumwa kutambua ulipwaji fidia ya ardhi unafuata sheria za nchini huku mkurugenzi wa jiji la Dodoma Bwana Godwin Kunambi akisema mvutano huu umetokana na madalali kununua ardhi katika eneo hilo wakiwa na lengo la kujinufaisha.