Back to top

Wananchi wajitolea kujenga kituo cha afya Isange Mbeya.

10 July 2018
Share

Zaidi ya wananchi 1200 wakazi wa kata ya Isange katika halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe wameanza ujenzi wa kituo cha afya kwenye kata yao kwa lengo la kusogeza karibu huduma za afya ili kuepusha vifo vya mara kwa mara hasa kwa akina mama wajawazito na watoto ambao wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilometa 15 kwenda kupata huduma kwenye kituo cha afya cha Kandete.

Halmashauri ya Busokelo mpaka sasa ina kituo kimoja tu cha afya kinachotoa huduma kilichopo eneo la Kandete, hali ambayo inasababisha wananchi waishio kata za pembezoni kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya kwenye kituo hicho, changamoto ambayo imewasukuma wakazi wa kata ya Isange kuanza ujenzi wa kituo chao cha afya ili kumaliza kadhia hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Busokelo, Eston Paul Ngilangwa  amesema serikali kuu tayari imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya na kwamba halmashauri yake kwa kushirikiana na wananchi watahakikisha kituo hicho kinakamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi oktoba mwaka huu.

Mbunge wa Busokelo, Mhe.Fred Atupele Mwakibete amesema jitihada za wananchi hao kutaka kujenga kituo cha afya cha kata yao zimeanza muda mrefu, lakini sasa anao uhakika wa kituo hicho kukamilika haraka baada ya rais Dkt.John Pombe Magufuli kuwaunga mkono kwa kuwapatia shilingi milioni 500 za ujenzi wa kituo hicho cha afya.