Back to top

Wananchi wakataa kujengewa kituo cha polisi Mbeya wakihofia vipigo

17 October 2018
Share

Wananchi wa kata ya Iyela jijini Mbeya wamekataa kupelekewa mradi wa ujenzi wa kituo cha polisi kwa madai kuwa polisi wamekuwa wakiwapiga na kuwaua hivyo wanataka mradi huo ubadilishwe kuwa Zahanati.

Wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, wananchi wa kata ya Iyela wamesema kwa muda mrefu hawana uhusiano mzuri na jeshi la polisi kutokana na jeshi hilo kuwapiga na kuwaua mara kwa mara na kwamba wanahofu wakijengewa kituo cha polisi vipigo na mauaji yataongezeka, hivyo bora wajengewe zahanati.

Pamoja na kuafiki mpango huo wa kubadili mradi wa kituo cha polisi kuwa kituo cha afya, baadhi ya vijana wa kata hiyo wamewataka wazazi kuwalea vizuri watoto wao ili wasiongeze uhalifu mitaani.

Akijibu ombi la wananchi hao, mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila  amesema anaafiki mawazo ya wananchi hao kujengewa zahanati badala ya kituo cha polisi huku akiahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya kwenye kata hiyo.