
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dkt.Angeline Mabula amewaonya wananchi walioingia kwenye migogoro ya matumizi ya ardhi na maeneo ya hifadhi nchini ambao maeneo yao yanafanyiwa tathmini na timu za wataalamu kutoongeza maeneo waliyopo sasa.
Dkt.Mabula ametoa kauli hiyo katika kijiji cha Lyamidati, kilichopo kata ya Kadoto Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakati Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanaoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 walipotembelea mkoa wa Shinyanga.
Kijiji cha Lyamidati ambacho wananchi wake wameingia kwenye mgogoro wa matumizi ya ardhi na eneo la hifadhi kinapakana na msitu wa hifadhi wa Nido ambapo baadhi ya vitongoji vipo ndani ya hifadhi huku uvamizi ukiwa kwenye maeneo ya makazi, kilimo pamoja na shughuli za ufugaji ndani ya hifadhi .
Katika eneo hilo Kaya 78 kati ya 170 za kijiji chote zipo ndani ya msitu huku vitongoji 3 navyo vikiwa ndani ya hifadhi.
Maelekezo ya Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta kwenye eneo hilo ni kufanyika tathmini ili vijiji ndani ya hifadhi virasmishwe, marekebisho ya mipaka yafanyike pamoja na kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
Waziri Mabula amesema baada ya kumegwa kwa eneo lenye migogoro ya matumizi ya ardhi lazima mipaka ipitiwe upya ili kujua eneo la hifadhi na lile litakalo baki kwa ajili ya matumizi ya wananchi na kusisitiza kuwa jambo hilo wananchi wanatakiwa kuwa nalo kichwani.
Amemsifia na kumshukuru Mhe.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa, pamoja na mabaya na uvamizi uliofanywa na wananchi kwenye maeneo ya hifadhi bado ameagiza kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kuzunguka na kuzungumza na wavamizi.
Mawaziri walioambatana na Dkt.Mabula katika ziara hiyo, walisistiza umuhimu wa kuwepo mipango ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo yaliyomegwa sambamba na maeneo ya hifadhi kutunzwa na kulindwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chana amewaambia wananchi kuwa, wizara yake inalo jukumu la kulinda. Kuitunza na kuihifadhi misitu yote nchini ambapo alisema hifadhi iliyoingia kwenye mgogoro wa matumizi ya ardhi katika kijiji cha Lyamidati Shinyanga ulishamegwa mara kadhaa hadi kubakia hekta 10,000.
Naye Waziri Ofisi ya Mazingira Muungano Khamis Hamza Chillo amewahimiza wananchi kuhakikisha wanapanda miti sambamba na kujiepusha katika uharibifu wa vyanzo vya maji.
Anthony Mavunde Naibu Waziri wa Kilimo amehimiza wataalamu kuhakikisha wanayawekea mipango ya matumizi ya ardhi maeneo yote yaliyomegwa ili kutengwa kwa ardhi kubwa kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta imehitimisha ziara yake katika mkoa wa Shinyanga na sasa inaendelea mikoa ya Mwanza na Mbeya.
