Back to top

Wananchi waliovamia pori la akiba Kijereshi watakiwakuondoka kwa hiari

19 July 2018
Share

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewapa siku 45 wananchi wanaoishi kinyume cha Sheria ndani ya kingo (bufer zone) za Pori la Akiba Kijereshi kuondoka kwa hiari yao wenyewe kabla ya kuanza operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu. 

Ametoa agizo hilo jana alipotembelea pori hilo katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu ikiwa ni muendelezo wa ziara zake mikoani kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi na kutatua changamoto zake.

Baada ya kushuhudia makazi na shughuli nyingine za kibinadam ndani ya pori hilo, Dk. Kigwangalla alitoa agizo hilo na kusema kuwa sheria za uhifadhi wa wanyamapori haziruhusu shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria pamoja na kingo zake (buffer zone) ambazo ni mita 500 kutoka kwenye mpaka halisi wa hifadhi husika.

"Mpaka itakapofika tarehe 31 mwezi ujao (Septemba) wananchi wote hawa wawe wameshaondoka eneo hili kwa hiari yao wenyewe, muwatangazie na mpime eneo hili vizuri muweke alama ili wajue ni wapi wanatakiwa kuondoka.

"Na ikifika tarehe 1 Septemba kama kuna watakaokuwa wamekaidi agizo hili, basi mfanye oparesheni maalum muwaondoe na msafishe kila kitu, ni lazima ifike mahali kila mmoja aheshimu sheria za nchi" alisema Dk. Kigwangalla kuuagiza uongozi wa pori hilo.

Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa muwekezaji wa hoteli ya kitalii ya Kijereshi Tented Camp kurudisha kwa Kamishna wa Ardhi hati miliki ya eneo lenye ukubwa wa hekta 464 lililopo ndani ya pori hilo kwa kuwa hati hiyo ni batili.

Alisema pori hilo lilianzishwa mwaka 1994 wakati muwekezaji huyo anadai kupewa hati ya kumiliki kipande hicho cha ardhi mwaka 1995. 

Aidha, ameagiza muwekezaji huyo aruhusiwe kuendelea kutoa huduma katika hoteli hiyo baada ya kusimamishwa kwa muda tangu mwaka jana na azingatie sheria na taratibu za uwekezaji ikiwemo kulipa ada na tozo mbalimbali.

Pori la Akiba Kijereshi ambalo lina ukubwa wa kilomita za mraba 65.72 linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA na lilipandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba mwaka 1994 kwa Tangazo la Serikali Na. 215 la terehe 10 Juni, 1994 na hiyo ni kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kiikolojia hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.