Back to top

Wananchi waomba uchunguzi wa Shilingi Milioni 85 za mradi Kyela.

09 August 2018
Share

Wananchi Kyela wameiomba serikali kuchunguza matumizi ya shilingi million.85 za mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wakidai umechakachuliwa.

Wananchi wa kijiji cha Mwaigoga, kata ya muungano wilayani Kyela wameiomba serikali kuu kuchunguza ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 85 ambazo zilitolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa skimu ya kilimo cha umwagiliaji katika kijiji hicho, wakidai kuwa mradi huo umechakachuliwa na fedha hizo zimeliwa na wajanja.

Wananchi hao  wa kijiji cha Mwaigoga wamesema mradi wa ujenzi wa skimu ya kilimo cha umwagiliaji wa Mpunga katika kijiji hicho ulipaswa kuanzia katika mto Mbaka na kutirirsha maji kuelekea kwenye mashamba yao, lakini maofisa wa halmashauri ya wilaya ya Kyela waliokuwa wakitekeleza mradi huo wameuchakachua kwa kutojenga banio kwenye mto Mbaka wala hawakujenga mifereji ya maji kuelekea kwenye mashamba yao na badala yake wameleta matanki manne ya kuhifadhia maji majumbani na kuwataka wananchi wayatumie kwa kilimo cha umwagiliaji hali ambayo imesababisha mradi huo kutokuwa na tija wala kukidhi mahitaji ya wananchi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mwaigoga Award Mikidadi ameiomba serikali ya awamu ya tano kuwasaidia ili mradi huo ujengwe upya huku asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Jitambue Lembuka inayojihusisha na utoaji wa elimu kwa wakulima wilayani Kyela ikidai kuwa utekelezaji wa mradi huo haukushirikisha wananchi.

Akizungumza na ITV kwa sharti la kutopigwa picha, mkuu wa wilaya ya Kyela, Cloudia Kitta amesema anaendelea kufuatilia hatma ya mradi huo kwa maofisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Kyela na kwamba atatoa tamko rasmi baada ya kujua ukweli kuhusu mradi huo.

 

 

 

.