Back to top

Wananchi wataka TASAF kuelekeza nguvu kwenye huduma za Afya na maji.

20 April 2021
Share

Wananchi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wamesema wilaya hiyo bado inaumasikini mkubwa kutokana na ukosefu wa huduma muhimu ikiwemo maji safi na salama, sambamba na uchache wa vituo vya kutolea huduma ya afya, hivyo wameomba mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF kipindi cha pili awamu ya tatu kuelekeza nguvu katika maeneo hayo ili wananchi waondokane na umasikini huo.

Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya wananchi walioudhuria kikao cha maelekezo kwa wawezeshaji kumi na tisa waliokuwa wakipewa mafunzo ili kutoa elimu kwa wananchi kutambua matakwa ya mradi wa TASAF kpindi cha pili awamu ya tatu.

Wamesema TASAF kipindi cha kwanza awamu ya tatu kimesaidia kiasi hivyo ni vema sasa sehemu ya fedha ielekezwa kwenye miundombinu ya maji na baadhi ya kata zenye changamoto ya huduma za afya ambazo zinachangia jamii kubwa kuzingirwa na umasikini.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji TASAF, Yasini Juma amesema TASAF awamu ya kwanza kipindi cha pili imesaidia kuondoa umasikini nchini kwa asilimia kumi, huku kaya masikini sana ukipungua kwa asilimia kumi na mbili.

Ameeleza lengo la serikali ni kuona awamu hii ya pili walengwa wote wanafikiwa nchi nzima lakini pia wasimamizi wa maradi huo wanafanya kazi kwa uandilifu pasipo udanganyifu wowote ili malengo ya kuondoa umasikini yaweze kufikiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu Moses Machali amesema yuko tayari kupambana na mtendaji yeyote katika wilaya hiyo ambaye atafanya udanganyifu katika mradi huo ambao serikali imewekeza fedha nyingi katika kupambana na umasikini.

Amesema anataka kuona kaya zitakazowekwa kwenye mpango huo zinavigezo lakini pia walengwa wa mradi huo ni wale walioainishwa kwenye mpango huo na si vinginevyo.