Back to top

Wanaosambaza taarifa za uongo juu ya mauaji ya watoto Njombe kubanwa.

06 February 2019
Share

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Kangi Lugola amesema watu 29 waliokamatwa kufuatia mauaji ya watoto mkoani Njombe ni wananchi wa kawaida hakuna viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini wala wafanyabiashara waliohusika katika tukio la mauaji ya watoto saba mkoani humo.

Akitoa taarifa ya serikali bungeni kuhusu mauaji na utekaji ya mauaji ya watoto yakihusisha imani za kishirikiana baada ya bunge kuomba taarifa ya serikali, Waziri wa mambo ya ndani Mh.lugola amewataka wananchi kuacha kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Njombe imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutuma timu ya wataalam wa upelelezi kwenda mkoani humo kufanya uchnguzi wa matukio hayo pamoja na kutumia falsafa ya ulinzi shirikishi kutoa elimu mashuleni kwa walimu ili kuwaelimisha wanafunzi waweze kuongeza umakini katika maeneo yao.

Mhe.Lugola amesema mkakati mwingine serikali imepanga kufanya sensa ya kuwatambua waganga wote wa jadi na kuaninisha walio na leseni na wasio kuwa na leseni ili kuwabaini waganga matapeli wanaopiga ramli chonganishi pamoja na kufanya doria katika maeneo mbalimbali ya misitu na nyumba za kulala wageni zilizopo pembezoni.

Aidha amesema si vyema kuhusisha mauaji hayo na shughuli za biashara na uzalishaji mali kwa kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza watu wasiohusika katika matukio ya uhalifu, na kusisitiza watu wote waliohusika ni wananchi wa kawaida wasiojihuisha na dini, siasa wala biashara.