Back to top

Wanunuzi wa pamba Shinyanga wapongezwa kwa kuwalipa wakulima mapema.

10 August 2020
Share

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Leo tarehe 10 Agosti 2020 amefanya ziara ya kikazi mkoani Shinyanga ambapo amekagua na kuridhishwa na hali ya ununuzi wa msimu wa Pamba kwa mwaka 2020/2021.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuchambua Pamba cha Afrisian, Aham, GAKI na Fresho Waziri Hasunga amewapongeza wamiliki wa kampuni hizo kwa mapokezi mazuri ya Pamba pamoja na kuwalipa wakulima kwa wakati.

Akizungumzia mfumo wa malipo ya Taslimu na Benki Amesema kuwa mifumo hiyo inaendelea kufanyiwa kazi ili kuona mfumo upi utakuwa na ubora zaidi kwa wakulima na wanunuzi.

Amesema kuwa serikali haitopanga bei elekezi ya mazao ya wakulima badala yake itaacha soko liamue. “Hatuwezi kumpangia bei mkulima kwani hatukumsaidia kuandaa shamba, kulima na hata kupalilia. Kwanini sasa hivi ameshavuna ndio tumuingilie hilo sio sahihi” Alisisitiza

Pia, Waziri Hasunga ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kusimamia kwa weledi mkubwa sekta ya kilimo jambo lililopelekea kuwa na ziada ya kutosha ya chakula.