Back to top

Waratibu elimu kata tokeni maofisini.

15 April 2019
Share

Serikali ya mkoa wa Simiyu imewaagiza waratibu elimu kata 133 wa mkoa huo kutoka maofisini na kwenda mashuleni kuwasimamia walimu wa madarasa ya awali,darasa la kwanza,la pili na la tatu na kuhakikisha wanafunzi wote wanawezeshwa katika stadi za KKK lengo likiwa ni kutekeleza agizo la serikali la kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayemaliza darasa la saba akiwa hajui kusoma kuandika na kuhesabu.

Kauli hiyo imetolewa kwa niaba ya uongozi wa mkoa wa Simiyu na katibu tawala wa mkoa huo Bw.Jumaane Sangi wakati akizungumza na waratibu elimu kata wa wilaya 6 zinazounda mkoa huo baada ya kupata elimu ya usimamizi wa stadi za ufundishaji na uchopekaji wa KKK katika mtaala mpya wa elimu ya msingi katika kituo cha elimu na mafunzo cha SHY-com mjini Shinyanga.

Nao baadhi ya waratibu kata wa mkoa wa Simiyu wamesema hatua ya serikali ya kuwaongezea ujuzi wa kusimamia maendeleo ya elimu itasaidia kupata wataalam mbalimbli na kuiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika ushindani wa soko la ajira duniani na kufikia uchumi wa kati mapema kupitia sekta ya kilimo,ufundi stadi na TEHAMA.

Kwa upande wake mratibu wa mafunzo kutoka wakala wa maendeleo ya uongozi wa elimu (ADEM) Bi.Gladys Masyole amesema tangu mafunzo ya stadi za elimu na uchopekaji wa KKK katika mtaala mpya wa masomo ya elimu msingi yaanze kutolewa nchini mwaka 2017 kumetokea mabadiliko makubwa kwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na ufaulu umeongezeka.