Back to top

Watu 2 wafikishwa Mahakama ya Kisutu kwa kuendesha biashara ya upatu

21 August 2019
Share

Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba ikiwemo kuendesha biashara ya upatu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai  ni Magdai Gothard na Halima Nsubuga.

Akisoma hati ya mashtaka  Agosti 21,2019 Wakili wa serikali Mwandamizi Wankyo Saimoni mbele ya Hakimu Mkazi  Mkuu Thomas Simba alidai  kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama kinyume na kifungu 384.

Alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Aprili Mosi na June 30,2017 Katika Mkoa na Jiji la Dar es salaam washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama na kutenda kosa.

Katika shitaka la pili alidaiwa kuwa washtakiwa hao kati ya Aprili Mosi na June 30,2017 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es salaam  walikusanya fedha kwa watu tofauti na kuwarudishia kwa faida.

Katika shitaka la tatu washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha Dola 394265 ,kati ya Aprili Mosi na June 30 washtakiwa wote kwa pamoja walielekeza fedha hizo kwenye akaunti  namba 3004211400319 kwa jina la Magdai Gothlard na Halima Nsubuga wakijua fedha hizo wamezipata kwa njia ya upatu.

Katika shtaka lingine washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha Dola 12309 kwa lengo la kuficha mahali fedha hizo zilipotokea.

Alidai kuwa Aprili 22,2017 ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es salaam washtakiwa hao walihamisha fedha hizo na kwenda kwenye akaunti 1002100721918 katika benki ya Equity  Uganda wakijua fedha hizo ni zao la fedha zilizopatikana kwa njia ya upatu.

Wakili Wakyo aliendelea kudai katika shtaka lingine la utakatishaji Aprili 24,2017 washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha Dola 29,086 kwa lengo la kuficha mahali fedha hizo zilipotoka wakati wakijua fedha hizo ni zao la kushiriki shughuli za upatu.

Wakili Wankyo alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine kwaajili ya kutajwa.

Wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai kuwa watawasilisha hoja ya uhalali wa hati ya mashtaka hivyo wanaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe ya karibu.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 30 mwaka huu,washtakiwa wamepelekwa rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji kutokuwa dhamana kwa mujibu wa sheria.