Back to top

Watu milioni 5.5 waambukizwa Corona ulimwenguni.

27 May 2020
Share

Idadi ya watu waliothibitika kuambukizwa virusi vya homa kali ya mapafu ya Corona duniani kote imepindukia na kufikia watu milioni 5.5, theluthi mbili ya watu hao wakiwa kutoka nchi za Ulaya na Marekani.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, kumekuwepo ongezeko maradufu la watu wanaougua maradhi ya COVID-19 yanayotokana na virusi hivyo vikali.

Maambukizi mapya yapatayo milioni moja yamethibitika katika muda wa siku 11 pekee kulingana na takwimu zilizopita ambazo zimetolewa na shirika la Afya Duniani Kote.

Barani Ulaya kumerikodiwa maambukizi ya watu milioni mbili na vifo 172,000, na nchini Marekani walioambukizwa virusi vya Corona ni zaidi ya milioni 1.6, huku idadi ya vifo ikiwa zaidi ya Watu 98,000.

Bara la Afrika limerikodi maambukizi takribani 116,000 ya Corona, maambukizi mengi yakiwa katika nchi tano ambazo ni Afrika Kusini, Misri, Nigeria, Algeria na Morocco.

Nchi hizo zinaongoza pia kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo wa Covid 19 ambavyo ni takribani watu 3,500 kwa bara zima la Afrika.