Back to top

Watuhumiwa saba wa kesi ya uhujumu uchumi waachiwa huru.

07 February 2019
Share

Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es salaam imewaachia huru watu saba baada ya Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kudai kuwa hana nia ya kuendelea kuwashtaki dhidi ya kesi ya uhujumu uchumi  ikiwamo kujiunganishia bomba la mafuta aina ya dizeli mali ya Mamlaka ya bandari Tanzania (TPA).

Washtakiwa hao waliachiwa chini ya kifungu cha 91 kidogo cha (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai   na Hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba.

Washtakiwa walioachiwa ni, Samwel Nyakirang'ani, Nyangi Mataro, Farijia Ahmed, Malaki Mathias, Christoms Angelus, Pamphile Koronko na Henry Fedrick.

Wakili wa serikali mwandamizi, Patrick Mwita  alidai kuwa DPP ameomba kuwaondolea mashtaka washtakiwa hao chini ya kifungu hicho kwamba hana nia ya kuendelea kuwashtaki dhidi ya tuhuma hizo.

Hakimu alisema mahakama yake haina pingamizi na ombi la DPP inawaachia washtakiwa saba kati ya 12.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano, wilaya ya Kigamboni, washtakiwa kwa pamoja walijiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoa katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali cha TPA.