Back to top

Wazazi na walimu watakiwa kuwafichua wanaouza dawa za kulevya.

15 October 2018
Share

Serikali imewaagiza walimu kwa kushirikiana wazazi nchini kuwafichua watu wanaosambaza dawa za kulevya katika baadhi ya shule za sekondari na vyuo kwa ajili ya kuwauzia wanafunzi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kufuatia baadhi ya wanafunzi katika shule za sekondari kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya.

Agizo hilo limetolewa na waziri wa elimu,sayansi na teknolojia Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako katika kongamano la wadau wa elimu lililofanyika wilayani Pangani kufuatia mkuu wa wilaya ya Pangani Zainab Issa kubainisha kuwa shule ya sekondari Funguni wanafunzi zaidi ya 10 wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya .

Katika kongamano hilo wadau wa elimu wa shule za sekondari wilayani Pangani wamemueleza mheshimiwa waziri Ndalichako kuwa wapo baadhi ya watendaji wa serikali za vijiji,askari pamoja na wataalam wa afya kuwa wanashirikiana na baadhi wazazi kuwaficha watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi bila kufikisha mashauri hayo katika vyombo vya sheria.

Kufuatia hatua hiyo mbunge wa jimbo la Pangani Mheshimiwa Jumaa Aweso amewaasa walimu kuacha majungu na badala yake wafanye kazi ili kukuza kiwango cha elimu.