Back to top

Waziri  Ummy azindua kituo cha huduma za simu kwa wananchi.

08 May 2020
Share

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua kituo cha huduma za simu kwa wateja ambacho kazi kubwa ni kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya ikiwamo magonjwa milipuko.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Ummy Mwalimu amesema kituo hicho kina uwezo wa kupokea simu 1000 kwa wakati mmoja na kuunganisha vituo vitano kwa wakati mmoja.

Amesema kazi ya kituo hicho ni kupokea maoni, taarifa, maswali na ushauri kuhusu masuala mabalimbali yanayohusu sekta ya afya na amewataka wananchi kupiga simu 199 ili wapate huduma na walioko nje ya nchi wanapaswa kupiga namba  0800110124.


Amewataka wananchi watakaopiga simu kuwa wastaarabu, kutumia lugha ya staha na kutoa taarifa sahihi ambazo zitasaidia Serikali  na Wizara ya Afya kuchukua hatua stahiki na kwa wakati. 

Amefafanua kwamba  kituo hicho kitatumika kutoa elimu na miongozo mbalimbali kuhusu masuala ya afya na kitakuwa na watalaamu 150 wakiwamo wataalamu wa afya, wauguzi na madaktari.

Amesema endapo Wizara ya Afya itaweza kutumia vizuri Tehama, itachangia changamoto mbalimbali zilizoko kwenye sekta ya afya, huku akiitaka jamii itambue kinga ni bora kuliko tiba na kwamba Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka minne na nusu imefanya vizuri katika masuala ya tiba na kinga.


Waziri wa Afya, amependekeza kituo hicho kipatiwe jina la ‘Afya Call Centre’ badala ya kituo cha huduma za simu ambacho kitakuwa kikishughulikia magonjwa yote.