Back to top

Waziri hasunga akagua maghala ya sukari Dar, atoa maagizo mazito.

16 May 2020
Share

Serikali imetangaza kuendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria  wafanyabiashara nchini wanaotumia uwepo wa ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID 19) kuhodhi kiasi cha sukari kinachokuwa kwenye mzunguko na kuuza kwa bei ya juu zaidi ya bei ya ukomo katika eneo husika ambayo ni kati ya Shilingi 2600 hadi 3200.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini.

Mhe Hasunga amesema kuwa serikali imeweka mbinu kali za kuwabaini wafanyabiashara hao na punde watakapobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ametangaza hali ya upatikanaji wa sukari nchini kuwa imeendelea kuimarika ambapo kufikia tarehe 16 Mei 2020 kiasi cha Tani 18,142 kimeingia nchini kati ya kiasi cha Tani 40,000 kilichoagizwa na wazalishaji wa ndani kwa ajili ya kuziba pengo la uzalishaji wa msimu wa mwaka 2019/2020.

Amesema kati ya kiasi hicho cha Tani 18,142 kilichoingizwa kiasi cha Tani 15,498 kimetolewa bandarini na mipakani na tayari kipo sokoni na kingine cha Tani 2,644 kipo katika hatua mbalimbali za kutolewa bandarini.

Amebainisha kuwa tarehe 16-22 Mei 2020 zitaingia Tani 7470, Tarehe 23-31 Mei 2020 zitaingia Tani 13,404, huku tarehe 1-4 Mei 2020 kiasi cha Tani 984 kitawasili nchini.