Back to top

Waziri Mkuu achukizwa na mamlaka ya maji kuongeza bili Maswa.

09 August 2019
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amekerwa na kitendo cha Mamlaka ya Maji wilayani Maswa kupandisha bili ya maji kutoka sh 5,000 hadi sh. 28,000 jambo ambalo amesema halikubaliki na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akutane na wahusika leo.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kumalija, wilayani Maswa mara baada ya kutembelea ghala la pamba la Chama cha Msingi cha Kumalija.

"Haiwezekani bili ikapanda kwa kiasi hicho. Hapo utakuwa unamsaidia mwananchi myonge au utakuwa unamnyonga.Bili haiwezi kupandishwa kwa asilimia kubwa kiasi hicho yaani imetoka shilingi elfu tano hadi shilingi elfu ishirini na nane."-Waziri Mkuu Majaliwa.

Ameongeza kuwa serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt.John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo upandishaji huo wa bili hauna tija kwa wananchi wanyonge.