Back to top

Waziri Mkuu aingilia kati michango ya bima vyuo vikuu.

09 August 2020
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa muda wa wiki moja kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kukutana na Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini ili kubaini vyuo ambavyo vimeshindwa kuwasilisha michango ya wanafunzi katika Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) licha ya wanafunzi kulipa fedha hizo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Agosti 9, 2020) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza kwa mwaka 2019/2020 wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania(TAHLISO) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi hao yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TAHLISO, Bw. Peter Niboye ambaye alisema kwamba kumekuwepo na ucheleweshaji wa vitambulisho vya bima ya afya unaotokana na baadhi ya vyuo kuchelewa kufikisha fedha NHIF.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagiza Menejimenti zote za vyuo vikuu nchini ziendelee kushirikiana kwa karibu na Serikali za Wanafunzi kwenye vyuo vyao ili waweze kushughulikia changamoto za wanafunzi kwa wakati.