Back to top

Waziri Mkuu akagua ukarabati wa Mv New Victoria.

09 August 2020
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ukarabati mkubwa wa meli ya MV New Victoria Hapa Kazi tu na kuagiza mamlaka inayosimamia ihakikishe kuwa kuanzia wiki ijayo meli hiyo inaanza kazi ya kusafirisha abiria na mizigo kwa kuwa ukarabati umekamilika na sasa inaendelea kukaa tu  hali ambayo ni hasara kwa Serikali.

Pia, Waziri Mkuu ametoa siku mbili kwa mamlaka inayohusika na utoaji wa kibali cha kuanza kazi kwa meli hiyo ihakikishe inatoa kibali hicho haraka na  ratiba ya safari itangazwe kwa sababu  Watanzania wanahamu  ya kuanza kuhuduiwa na meli hiyo.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Agosti 9, 2020 baada ya kukagua meli hiyo ambayo tayari imeshafanya safari ya majaribio  kwa  kusafirisha abiria kutoka Mwanza hadi Bukoba mkoani Kagera ambako ilirudi na abiria na mizigo.

Maeneo aliyokagua kwenye meli hiyo ni pamoja na vyumba vya abiria vikiwemo vyumba maalumu kwa ajili ya huduma za mama na mtoto, chumba cha kuongozea meli, vyumba vya migahawa na chumba cha injini.

Baada ya kukagua meli ya MV New Victoria Hapa Kazi Tu, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa chelezo pamoja na meli mpya na alieleza kuwa ameridhishwa na kazi inayoendelea kufanyika na amewataka Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali yao.