Back to top

Waziri Mkuu aridhishwa na kasi ya ujenzi reli ya kisasa Dar, Moro.

07 August 2020
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kueleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi ambao umefikia asilimia 87.

Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu ya usafiri wa reli, anga, maji na barabara ili kutoa fursa kwa wananchi kuchagua aina ya usafiri wanaohitaji kuutumia pia kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha biashara baina ya Tanzania na Mataifa mengine.

Waziri Mkuu ambaye alianza ziara hiyo kwa kukagua ujenzi wa jengo la stesheni ya Dar es Salaama ambalo linamuonekano wa madini ya Tanzanite, amesema ujenzi unaendelea vizuri na amemtaka mkandarasi akamilishe kwa wakati kwani Watanzania wanasubiri kwa hamu.  

“Hii ni mara yangu ya tatu nafanya ukaguzi wa ujenzi wa mradi huu na wakati wote naridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake ambao unajengwa kwa kutumia fedha za Watanzania na asilimia 90 ya wafanyakazi wanaojenga mradi huu ni Watanzania.”

Waziri Mkuu amesema Watanzania waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imejipanga katika kuendelea na kuimarisha ujenzi wa miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.” Na huu ndio utekelezaji wa maelekezo ya CCM iliyoyatoa kwa Serikali yake.”

Akiwa katika stesheni ya Ruvu mkoani Pwani, Waziri Mkuu alipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi yakiwemo ya wakulima kunyanyaswa na wafugaji kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao hivyo kuwafanya wakose chakula.