Back to top

Waziri Mkuu awataka watanzania kuwalinda vijana.

17 April 2021
Share

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuhusika na ulinzi wa watoto kwa kuweka mipango itakayoondoa mazingira yanayowafanya vijana balehe kuwa na tamaa ya vitu na kushawishika kujiingiza kwenye ngono katika umri mdogo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Aprili 17, 2021) wakati wa uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe katika ukumbi wa Hoteli ya Morena, jijini Dodoma.

 Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amesema programu za kuelimisha Vijana Balehe kuhusu madhara ya kuanza ngono mapema ziandaliwe ili washiriki kikamilifu katika masomo na masuala mengine ya maendeleo kwa kuwawezesha kupata taarifa sahihi.

Waziri Mkuu amesema takwimu za Elimu Msingi Tanzania (BEST - 2020) zimeonesha kuwa jumla ya watoto 1,135 katika shule za msingi na 5,340 katika shule za sekondari waliacha shule kwa sababu ya mimba hadi Desemba, 2020”.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha changamoto zinazolikabili kundi hilo zikiwemo za magonjwa ya kuambukizwa, upungufu wa taaluma sahihi za kujiajiri na kuajiriwa, matumizi ya dawa za kulevya, ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wadau wote wa masuala ya afya na maendeleo ya vijana balehe nchini kubuni na kuandaa afua zilizofanyiwa utafiti zenye kuleta matokeo chanya katika kutokomeza mimba za utotoni.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Afya ihakikishe kuwa vijana balehe watakaothibitika kuwa na maambukizi ya VVU wanaunganishwa na huduma za tiba na matunzo ili wawe na afya njema itakayowawezesha kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku.