Back to top

Waziri Mkuu awatolea uvivu wapotoshaji CORONA.

21 March 2020
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonya juu ya upotoshwaji na utoaji holela wa taarifa kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababisha na virusi vya Corona (COVID 19) unaofanywa na watu mbalimbali nchini.

Amesema kuanzia sasa taarifa hizo zitatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ikilazimika zitatolewa na Waziri Mkuu na ikilazimika sana zitatolewa na viongozi wakuu wa nchi ili kuepusha mikanganyiko.

“Watu wote wanaopotosha umma na kuleta taharuki kuhusu ugonjwa wa corona badala ya kuelimisha namna ya kujikinga, wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema licha ya hali ya maambukizi ya corona nchini kutia matumaini, viongozi hao hawana budi kupeana taratibu za namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

“Wakuu wa mikoa kila mmoja ahakikishe eneo lake linakuwa salama na endapo kutakuwa na mgonjwa tumieni zahanati ambazo bado hazijaanza kutumika kwa ajili ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa Corona,” amesema.

Amewataka wakuu hao wa mikoa waimarishe utoaji wa elimu kwa umma na ikiwezekana watumie magari ya matangazo ili wananchi waelewe athari za ugonjwa huo na namna ya kujikinga pamoja na kuwaondolea hofu ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.

Pia amewataka watumie redio za kijamii katika maeneo yao kutoa elimu kwa umma juu ya kujikinga na ugonjwa huo na wasimamie maeneo ya utoaji huduma kama vituo vya mabasi na kuhakikisha kila abiria anakaa kwenye kiti.

“Nendeni kwenye maeneo ya mikusanyiko, vituo vya mabasi kutoa elimu kwaumma na kuwaondoa hofu Upande wa maofisini, viwandani na kwenye mgodikuwe na utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyakazi kila siku asubuhi watumie hata robo saa kabla ya kuanza kazi waelekezwe namna ya kujikinga.”

Waziri Mkuu amesema kwa wanaoishi katika maeneo ya makambi, viongozi wao waelekezwe namna ya kutoa elimu ya kujikinga na corona na pia
wadhibiti utorokaji na Serikali kwa upande wake inaendelea kuimarisha udhibiti mipakani, uwezo wa kupima sampuli na upatikanaji wa vifaa.

Amewataka wakuu hao wa mikoa, wawashirikishe wakuu wa wilaya kwenye mikoa yao ili wasimamie utekelezaji wa maagizo hayo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu hao wa mikoa wahakikishe wanawafuatilia na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote watakaobainika kuongeza bei kwa bidhaa ambazo zinatumika katika udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Kuhusu viongozi wa dini, Waziri Mkuu amewaomba waendelee kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha waumini wao wote kuzingatia tahadhari za ugonjwa huu. Pia waendelee kuliombea Taifa.