Back to top

Waziri Mpina aagiza kuandaliwa muongozo wa kusimamia chanjo za mifugo

20 January 2019
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Mpina amemuagiza Mkurugenzi wa huduma za mifugo kushirikisha wadau wengine wa sekta hiyo ikiwemo chuo kikuu cha sokoine na vituo vya utafiti kuandaa mwongozo shirikishi wa pamoja kusimamia chanjo toka kuzalishwa, kununuliwa hadi kusambazwa ili wananchi wapate faida ya kuwa na kituo cha chanjo nchini.

Waziri Mpina amesema hayo baada ya kuitembelea taasisi ya kitaifa ya chanjo ikiwemo kituo cha chanjo kitaifa kilichopo Kibaha mkoani Pwani na kile cha rufaa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Temeke Dar es Salaam pamoja na wakala wa maabara za Vetenari Tanzania ambapo akaagiza chanjo zote ni lazima zizalishwe nchini ili kuondoa gharama kubwa ya uagizaji chanjo toka nje. .

Waziri Mpina akataka mahitaji muhimu katika vitengo hivyo kuandaliwa mapema ili ya dharura yaingizwe kwenye bajeti na kuahidi kuzindua utoaji chanjo mpya ya majaribio ya ugonjwa wa mapafu ya ng'ombe mkoani Tanga, na kumuomba rais kuzindua maabara inayoendelea kujengwa ili kutenganisha chanjo za magonjwa yanayoenezwa na virusi na yale yatokanayo na bakteria huko kibaha kutokana na umuhimu wake, huku mkurugenzi wa mifugo Dkt.Hezron Nonga akasema magonjwa mengi wanayokinga kwa chanjo yanaambukiza binadamu na mifugo.