Back to top

Wema Sepetu kusomewa maelezo ya awali Februari 21,mahakama ya Kisutu

13 February 2019
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 21, mwaka huu kumsomea maelezo ya awali( PH) msanii wa Filamu nchini, Wema Sepetu.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa shauri hilo kukamilika na hivyo upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa hayo.
Wema ambaye alikuwa Miss Tanzania mwaka 2006,  anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mitandaoni ya kijamii.

Wakili wa Serikali, Glori Mwenda, ameieleza mahakama , Februari 13, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonda, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Kasonde baada ya kusikiliza Maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, mwaka huu ambapo upande wa mashtaka utamsomea PH.

Wema ambaye anatetewa na wakili, Ruben Simwanza, alifikishwa  kwa mara ya kwanza Kisutu,  Novemba Mosi, 2018, kujibu shtaka hilo.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, Wema anadaiwa Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.