Back to top

WHO yaridhia chanjo ya Corona AstraZeneca kupelekwa mataifa masikini.

16 February 2021
Share

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeridhia chanjo ya virusi vya Corona ya AstraZeneca kuanza kupelekwa kwenye mataifa masikini, baada ya kuithibitisha kwa dharura.

Mataifa ya kipato cha chini na cha kati yanatarajiwa kupata dozi ya kwanza ya chanjo hiyo mwishoni mwa mwezi Februari, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kimataifa wa mgawanyo wa chanjo, COVAX.

Shirika hilo linatarajia kupeleka dozi milioni 336 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka na hadi bilioni 2 ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba.

Kulikuwa na matarajio kwamba mpango huo wa COVAX ungeanza sambamba na utoaji wa chanjo kwa mataifa tajiri.

Hata hivyo, miezi miwili baada ya mataifa hayo kuanza, hakuna chanjo hata moja iliyoanza kutolewa miongoni mwa watu bilioni 2.5 waliopo kwenye mataifa masikini zaidi yapatayo 130.