Back to top

Wizara ya Mifugo yaagizwa kuboresha utoaji elimu ya ufugaji.

08 August 2020
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ihakikishe inaboresha utoaji wa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji ili kuiwezesha mifugo yao kuwa na ubora na uzito mkubwa badala ya mifugo ya aina hiyo kuonekana kwenye maonesho pekee.

"Mara nyingi ng’ombe wenye uzito wa kilo mia nane, mia tisa nawakuta kwenye maonesho tu lakini hatuwaoni kwa wafugaji. Hawa anawatunza nani na kwa nini tusiwaambie wawatunze kama mnavyowatunza. Lazima tuwe na ng’ombe wanaofugwa na wafugaji wenye uzito huo, hivyo wafundisheni namna ya kuwatunza"

Waziri Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt.John Pombe Magufuli katika sherehe hizo ametoa agizo hilo alipotembelea banda la Wizara hiyo katika kilele cha Maonesho ya Kilimo na Sherehe za wakulima Nane Nane Kitaifa kwenye Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu, Kauli mbiu ya sherehe hizo kwa mwaka huu ni 'Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020'.

"Nimetembelea baadhi ya mabanda kwenye viwanja hivi vya Nyakabindi na nimeona bidhaa nyingi zinazotokana na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, huu ni ushahidi tosha wa mchango wa sekta ya kilimo katika kufikia uchumi wa kati. Tukumbuke kwamba safari yetu ya kujenga uchumi wa viwanda inaendelea"

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali walioitikia wito wa Serikali kwa kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata, kusindika na kutengeneza bidhaa zinazotokana na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesema kupitia maonesho hayo ya 28 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993, wakulima, wafugaji, wavuvi, wanaushirika na wajasiriamali hupata fursa ya kuonesha na kujifunza matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji wa uhakika wa chakula sambamba na kukidhi mahitaji ya viwanda na masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Binafsi, nimefurahishwa na ubora wa bidhaa hizo, hakika mmejitahidi sana. Nimeridhika pasipo shaka kuwa wananchi waliotembelea viwanja hivi, nao wamepata fursa ya kujifunza na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.”

Amesema kuwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ni malighafi muhimu kwenye viwanda na huchangia asilimia 65 ya malighafi zinazohitajika viwandani. Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zimeendelea kutoa fursa nyingi za ajira kuliko sekta zote na asilimia 58 ya Watanzania wameajiriwa na kujiajiri katika sekta hizo.

Waziri Mkuu amesema kilimo ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa na katika  kipindi  cha  miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka sh. trilioni 25.2 mwaka 2015 hadi sh. trilioni 29.5 mwaka 2019.