Back to top

Zaidi ya akinamama 40 mkoani Kagera wapoteza maisha wakijifungua.

12 September 2018
Share

Zaidi ya akinamama 40 mkoani Kagera wamefariki dunia wakati wa kujifungua katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani humo na katika ngazi ya jamii katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kutokwa na damu nyingi wakati na baada ya kujifungua, uambukizo, kifafa cha mimba na upungufu wa damu.

Takwimu za vifo hivyo zimetolewa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Kagera Dkt. Marco Mbata, wakati akielezea mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa USAID Boresha afya unaofadhiliwa na shirika la misaada la maendeleo la watu wa marekani USAID, ambapo kuhusu vifo vya watoto wachanga amesema hadi kufikia Juni mwaka huu vilikuwa 365, kati ya hivyo vifo 270 vilitokana na watoto kuzaliwa wakiwa tayari wamefia tumboni, amesema idadi hiyo imepungua ukilinganisha na vifo 1007 vya watoto wachanga vilivyotokea mwaka jana 2017.

Akizungumzia huduma za dharura za upasuaji na damu salama zinazotolewa katika vituo 19 mkoani humo, Dkt. Mbata anaelezea hatua zinazochukuliwa na wadau kwa kushirikiana na timu za uendeshaji wa huduma za afya mkoani humo ( RHMT ).

Mahitaji ya damu katika mkoa wa Kagera kwa mwaka ni Chupa 24,580. Kabla ya mradi wa USAID Boresha afya kuanza mkoani humo mwaka 2016/2017, ukusanyaji wa damu ulikuwa ni chupa 6,622. Hata hivyo kuanzia Oktoba mwaka jana hadi kufikia Agosti mwaka huu mkoa huo umefanikiwa kukusanya chupa 11,257 za damu salama na kati ya hizo chupa 2007 sawa na asilimia 18 zimekusanywa kwa ushirikiano na mradi huo.