Back to top

Zaidi ya maduka 20 ya viuatilifu yamefungwa kwa kuuza viuatilifu feki

23 June 2018
Share

Taasisi ya utafiti wa viuatilifu nchini, TPRI, imeyafungia maduka zaidi ya 20 ya kuuza viuatilifu katika wilaya za Mbeya na Kyela mkoani Mbeya baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza na kuyakuta maduka hayo yakiwauzia wakulima viuatalifu feki ambavyo havijasajiliwa nchini, huku baadhi ya wauzaji wakiwa hawana mafunzo maalum ya kuwawezesha kutoa maelezo kwa wakulima kuhusu viuatilifu wanavyouza.

Taasisi ya utafiti wa viuatilifu nchini, TPRI, kanda ya nyanda za juu Kusini yenye ofisi zake Jijini Mbeya, imefanya ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo ya Inyara na Uyole wilayani Mbeya kabla ya kuhamia katika miji ya Ipinda na Kasumulu wilayani Mbeya ambako wamekuta wafanyabiashara wenye maduka ya viuatilifu wakiwa hawana vibali vya kuuza viuatilifu huku pia kukiwa  na makosa mbalimbali yanayohatarisha usalama na ubora wa viuatilifu kwenye maduka hayo na ndipo uamuzi wa kuyafungia ukachukuliwa.

Wakizungumza baada ya kufungiwa maduka yao, baadhi ya wamiliki wa maduka hayo wameitaka TPRI kuelekeza udhibiti wa viuatilifu feki kwa wasambazaji makubwa ambao ndio wanaowauzia wenye maduka madogo.

Katika hatua nyingine wauzaji wa viuatilifu walio na maduka katika mji mdogo wa Kasumulu wilayani Kyela ambapo ni mpakani mwa Tanzania na Malawi, wameiomba serikali kutoa vibali vya vya kuruhusu viuatilifu vya aina moja ambavyo vimesajiliwa Tanzania na Malawi kuuzwa pande zote za mpaka bila vikwazo ili kuwawezesha wafanyabiashara wa watanzania kumudu ushindani wa biashara ya mpakani.