Watoto wanaoishi katika vijiji vilivyokumbwa na mafuriko katika wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya utapiamlo kutokana na ukosefu wa lishe bora.
Hayo yamebainishwa na daktari wa watoto kutoka Taasisi ya afya KCMC Dkt Jonstone George wakati wa zoezi la kutoa huduma za afya bure na vipimo vya magonjwa mbalimbali kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano kwenye vijiji vitatu vilivyokumbwa na mafuriko katika wilaya ya Mwanga.
Katika zoezi hilo ambalo limeendeshwa na madaktari kutoka hospitali ya rufaa ya KCMC na wanafunzi wa Chuo kikuu cha tiba KCMC jumla ya watoto elfu tatu (3,000)wamepatiwa huduma za afya na wazazi kupewa elimu ya lishe kwa watoto hao ambao tayari wameabinika kuwa na viashairia na ugonjwa wa utapiamlo.
Akizungumza wakati wa kutoa huduma za afya kwa watoto katika zahanati ya Kifaru Mhadhiri wa Chuo kikuu cha tiba KCMC Dk Florida Muro amesema lengo la kutoa huduma za vipimo kwa watoto wa vijiji hivyo ni pamoja na kuhakikisha afya zao zinakuwa salama kwa kuwa watoto ndiyo wanaoathirika zaidi wakati wa majanga kama mafuriko yanapotokea.
Kwa upande wake Muuguzi Mfawidhi zahanati ya kifaru na baadhi ya wanawake wamesema upatikanaji wa chakula kwa baadhi ya maeneo ni changamoto kubwa hali ambayo inasababisha watoto kukosa lishe bora.