Back to top

Zitto aachiwa kwa dhamana, asomewa mashtaka matatu ya Uchochezi.

02 November 2018
Share

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Mh.Zitto Kabwe ameachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya shilingi milioni 10, kitambulisho cha taifa na mdhamini mmoja, ikiwa ni saa chache tu baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi kati ya wananchi na polisi.

Leo Novemba 02,2018, Wakili wa Serikali Tumaini Kweka ameiambia Mahakama, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi kwamba mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo Oktoba 28, alipokuwa akifanya mkutano na wanahabari.

Ikumbukwe tu kwamba amri ya kukamatwa na polisi kwa Zitto Kabwe ilianza kutolewa na polisi Kigoma ikimtaka awasilishe vielelezo juu ya kauli aliyokuwa kaitoa mbele ya wanahabari Oktoba 28, akieleza kwamba anazotaarifa juu ya zaidi ya wananchi 100 kuuawa katika mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Baada ya wito wa polisi Kigoma, Jeshi la Polisi Dar liliweza kumkamata na kumshilikia Kiongozi huyo wa ACT - Wazalendo ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini kwa siku tatu tangu siku Jumatano kuhusiana madai kuwa wananchi zaidi ya 100 waliuawa katika mapigano kati ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Kesi hiyo sasa imeahirishwa mapaka Novemba 12, 2018.