Back to top

Zoezi la kufufua visima liwe endelevu

10 November 2022
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amekagua visima vya dharura vinavyosafishwa, kufufuliwa na kuunganishwa katika mfumo wa usambazaji maji kwa wananchi na kuagiza zoezi hilo pamoja na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali liwe endelevu.

Mheshimiwa Majaliwa amekagua visima katika eneo la Tabata Relini na Mwananyamala Komakoma jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi, Novemba 10, 2022), ambapo ameshuhudia usafishwaji wa kisima pamoja na zoezi la usambazaji maji.



Visima hivyo ni miongozi mwa visima 197 vilivyochimbwa na Serikali mkoani Dar es Salaam ambapo kwa sasa 160 vimefufuliwa na kutoa lita milioni 29.4 kwa siku, Maji hayo yameunganishwa katika mfumo na hivyo kupunguza changamoto ya maji.

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Bonde la Wami Ruvu pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) waendelee kufanya tafiti kubaini maeneo yenye maji mengi na kuchimba visima na kuyaingiza katika mfumo.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda maeneo yote yenye vyanzo vya maji pamoja na kuyatumia vizuri maji yanayopatikana ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji hususani katika kipindi hiki cha ukame.