Back to top

Petroli na Dizeli zakamatwa zikiuzwa katika makazi ya watu Dodoma

19 September 2019
Share

Jeshi la polisi mkoa wa Dodoma limekamata jumla ya watuhumiwa 45 kwa kosa la kufanya biashara ya mafuta katika makazi ya watu pamoja na kando kando ya barabara bila ya kuwa na leseni kitendo ambacho ni hatari kwa usalama wa maisha yao ambapo zaidi ya lita elfu nne za mafuta ya petroli na dizeli zimekamatwa katika msako mkali unaoendelea wilaya zote za mkoa wa Dodoma

Akizungumza jijini Dodoma kuhusu misako mbalimbali inayoendelea kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma kamishna msaidizi wa polisi SACP Gilles Muroto amesema lengo la operesheni hiyo ni kukomesha biashara hiyo ya mafuta ambayo kwa sasa imekuwa ikishamiri katika makazi ya watu na kuhatarisha maisha  huku akipiga marufuku wananchi wanaovunja sheria kwa kuuza mafuta katika makazi yao.

Aidha kamanda Muroto amesema kupitia misako mbalimbali inayoendelea katika makao makuu ya nchi Dodoma wamefanikiwa kukamata pombe haramu ya moshi pamoja na madawa ya kulevya aina ya bangi ambapo amewataka wananchi kuhakikisha hawashirikiana na wahalifu na badala yake watoe taarifa za vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.

Wakizungumza na ITV kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wametaka operesheni hiyo kuwa endelevu ili kuwabaini watu wanaouza mafuta katika makazi ya wananchi ambapo wamesema wapo tayari kushirikiana na jeshi la polisi katika kufichua vitendo vya uhalifu