Back to top

Serikali kujenga pampu ya gesi mkoani Mtwara

19 September 2019
Share

Serikali imesema inatarajia  kujenga kituo cha kujaza gesi kwenye magari  mkoani Mtwara kitakachogharimu dola za kimarekani bilioni moja  ifikapo mwezi wa kumi na mbili mwaka huu na maandalizi tayari yameanza.

Waziri wa nishati Dkt.Merdadi Kalemani amesema hayo mkoani Mtwara huku akisisitiza  tayari mazungumzo na chuo cha ufundi  VETA mkoani Mtwara  yameanza ili kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa pampu hiyo ya kujaza gesi kwenye magari.
Amesema lengo la serikali ni kuona wananchi wanaendesha magari yanayotumia gesi ambayo gharama yake ni nafuu kwa asilimia sabini ukilinganisha na magari yanayotumia mafuta ya dizel na petroli.

Amesema kwa sasa yapo magari takribani miambili na hamsini yanayotumia mfumo wa gesi katika mikoa ya Dar es Salaam, na  Pwani hivyo lengo la serikali ni kuona  wananchi wake wanaendesha magari yenye mfumo wa kutumia gesi ili kupunguza gharama.

Hata hivyo amesema kwa sasa serikali  itaanza kujenga miundombinu hiyo ya gesi katika mikoa saba ambapo tayari imetenga shilingi bilioni tano nukta sita kwa ajili ya kununua miundombinu kama vile magari na matenki makubwa  ambayo yatajengwa kwenye baadhi ya mikoa kama vile Dodoma, Arusha, Mwanza , na  Iringa.