
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega, ametaka wafugaji kumilikishwa ardhi na kupatiwa hati kwa ajili ya shughuli za ufugaji.
Ulega ametoa kauli, mkoani Songwe kwa nyakati tofauti wakati Kamati ya Mawaziri 8 wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975, ilipozungumza na uongozi wa mkoa wa Songwe pamoja na kutembelea wananchi wa kitongoji cha Ikanka kijiji cha Itumba wilayani Ileje.
Amesema wakati ikisisitizwa ardhi inayomegwa kwenye maeneo mbalimbali ya hifadhi kupangiwa mipango ya matumizi ni wakati muafaka sasa kwa ardhi hiyo nayo kutolewa kwa shughuli za mifugo na wamiliki wake kupatiwa hati.
Ameongeza kuwa hatua ya kuyapatia mashamba mifugo hati mbali na kuwasaidia wafugaji kuwa na umiliki wa ardhi lakini itawazuia kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, sambamba na kuwatambua kwa urahisi ambapo amesema kwa sasa inakuwa vigumu hata wafugaji kukopesheka wakati ni matajiti.

