
Waziri Mkuu mpya wa Italia Giorgia Meloni, ameahidi kuwazuia wahamiaji kutoka Afrika kuvuka kwa kutumia boti, wakati tahadhari ikitolewa kuwa zaidi ya watu 1,300 wamepata matatizo katika bahari ya Mediterania.
Meloni amesema serikali yake, yenye siasa kali zaidi za mrengo wa kulia tangu vita vikuu vya pili vya dunia, inataka kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu hasa kwa kuzuia wahamiaji kutoka Libya iliyokumbwa na mgogoro.
Waziri Mkuu huyo amesisitiza kuwa ni wakati wa kuzuia hatua ya wasafirishaji kuamua aina ya watu wanaofaa kuingia Ulaya, huku waziri wake mpya wa mambo ya ndani akisema huenda akazuia meli za misaada kuwapeleka wahamiaji nchini Italia, na kufufua sera ya mwaka 2019 iliyozusha utata.
