
Serikali imesitisha kwa muda wa miezi mitatu, zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za Kielektroniki wakati ikiendelea na tathmini ambayo itawezesha kutoa muongozo wa namna bora zaidi ya kutekeleza zoezi hilo.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki na kuzuka kwa moto katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.
Hata hivyo, amesema serikali haijasitisha malipo kwa ajili ya huduma hiyo bali imesitisha zoezi linalolalamikiwa ili kuipa nafasi serikali kupitia Wizara ya Mifugo kufanya tathmini ya upungufu wa kikanuni yaliyowekwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo vizuri kwa kushirikisha wadau wa mifugo.
Amesema bei elekezi ya kuweka hereni za kielektroniki kwa mnyama mmoja ni shilingi 1,750 kwa ng'ombe na punda na shilingi elfu moja kwa mbuzi na kondoo, gharama ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wafugaji kuwa ni kubwa tofauti na uhalisia.
Mhe.Majaliwa amesema sertikali imesikia hoja za wafugaji kuhusu upungufu wa kanuni, usimamizi wake na utekelezaji wake na gharama kubwa za uwekaji hereni za kielektroniki na inaona kuna haja ya kufanya upya tathmini ya zoezi hilo.
