
Viongozi mbalimbali wa Umma wameipongeza Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kitendo cha kuanzisha huduma ya kujaza na kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao (Online Declaration System- ODS).
Kwa nyakati tofauti Viongozi hao wametoa pongezi hizo wakati walipotembelea banda la ofisi hiyo, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Akizungumzia mfumo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Bw. Suleiman Msumi amesema mfumo ni mzuri kwani Kiongozi anaweza kujaza taarifa zake akiwa popote pale , pia umepunguza gharama na muda na kuongeza kuwa mfumo ni rafiki katika utunzaji taarifa zilizopo kwenye Tamko kulinganisha na kuwasilisha Tamko kwa njia ya nakala ngumu ambapo ni rahisi kupotea na taarifa ambazo ni siri kuvuja kwa urahisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Uchapishaji na Huduma za Maktaba Katika Kurugenzi ya Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Bw. John Kabale amesema mfumo huo ni rafiki kwa Viongozi na kuongeza kuwa yeye alijaza taarifa zake akiwa nyumbani na alipopata changamoto aliwasiliana na Afisa TEHAMA kwa msaada mpaka kukamilisha kujaza na kuwasilisha Tamko lake.
Kiongozi mwingine aliyepongeza matumizi ya kujaza Tamka la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao ni Dkt Adolar Duwe ambaye ni Meneja Usimamizi Rasilimaliwatu na Utawala kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Dkt. Duwe amesema mfumo wa ODS ni rafiki kwake maana alijaza na kuwasilisha Tamko lake akiwa ofisini kwake akiendelea na majukumu mengine na akipata muda anajaza taarifa zake na kuhifadhi na kuendelea hatua kwa hatua mpaka kuwasilisha Tamko lake kwa wakati na kupongeza hatua kubwa wanayofanya Sekretarieti ya Maadili kwa kusimamia maadili kwa Viongozi wa Umma nchini.