Back to top

MAJALIWA:WAKUU WA SHULE, MADEREVA ZINGATIENI USALAMA WA WANAFUNZI

25 April 2024
Share

Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa, amewataka wamiliki wa shule na madereva wa mabasi yanayotoa huduma za usafiri kwa wanafunzi wajiridhishe kuhusu njia wanazopita ili kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa wanafunzi wanaowabeba katika vyombo vya usafiri.

“Wazazi, Walezi na Jamii ya Watanzania kwa ujumla tushiriki kikamilifu katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanapokwenda na kurudi Shuleni wakati wote hususani katika kipindi cha mvua.”.Majaliwa.

 Kadhalika amesema kwa kuwa Serikali imetoa maelekezo ya kufunga shule zilizoathiriwa na mafuriko, halmashauri na wamiliki wa shule zisizo za Serikali waweke utaratibu wa kufidia muda wa vipindi ili kukamilisha kalenda ya muhula kama ilivyopangwa.

Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Aprili 25, 2024) wakati akitoa taarifa ya serikali kuhusu changamoto  za hali ya hewa bungeni jijini Dodoma.

Pia, amezitaka Taasisi za Serikali ziendelee, kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau kutekeleza majukumu yaliyoanishwa katika Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El-Nino pamoja na mipango ya kisekta ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Aidha, amewataka Wakuu wa mikoa na wilaya, maafisa tarafa, watendaji kata, mitaa na vijiji wasimamie ipasavyo usafi katika maeneo yao na kudhibiti utupaji taka ovyo unaosababisha kuziba kwa mitaro badala ya kusubiri usafi unaofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.