Tanzania yatoa msamaha kwa wahamiaji haramu Elfu Moja kutoka Ethiopia

Serikali ya Tanzania imetoa msamaha kwa wahamiaji haramu zaidi ya Elfu moja waliofungwa katika magereza mbalimbali nchini kwa makosa ya kuingia nchini kinyemela na imeitaka Ethiopia kutoa ushirikiano ili kudhibiti raia wanaoingia nchini bila kufuata utaratibu.

Msamaha huo umetolewa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli wakati akimkaribisha nchini Rais wa Ethiopia Bibi Sahle-Work Zewde akisema amechukua uamuzi huo ili kujenga ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Rais Magufuli pia amewakaribisha wawekezaji kutoka Ethiopia kuja kuwekeza nchini katika sekta ya mifugo, ikiwemo kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ili Watanzania wanufaike na mifugo yao.

Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutoa msamaha kwa wahamiaji haramu na ameahidi serikali yake kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji, biashara pamoja kukuza Lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu.

Kuhusu sakata la serikali ya Ethiopia kuinyang'anya viwanja Tanzania kwa kushindwa kuviendeleza, Rais Sahle-Work Zewde ameahidi kuirudishia Tanzania viwanja hivyo ili kujenga ofisi za ubalozi.

Rais Sahle-Work Zewde tayari ameondoka nchini Tanzania leo kurejea Ethiopia.