Back to top

PAC YAIPONGEZA WIZARA YA ARDHI UTEKELEZAJI MRADI

28 March 2024
Share

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika halmashauri ya Mji wa Nzega mkoa wa Tabora.

Pongezi hizo zimetolewa wilayani Nzega na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Japhet Hasunga wakati wa ziara ya Kamati yake kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji mradi wa LTIP kwenye halmashauri ya Mji wa Nzega mkoani Tabora.

Mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Mji wa Nzega umepewa lengo la kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 na kuongeza alama za msingi za upimaji 14.

Amesema, Mhe.Rais ameamua kutoa fedha nyingi za mradi wa LTIP na Bunge kuidhinisha ambapo kwa upande wa halmashauri ya Mji Nzega kiasi cha Shilingi Bilioni 1.4 kimeidhinishwa kwa ajili ya Kata tano hivyo wananchi watumie fursa ya kutambuliwa maeneo yao na hatimaye kupatiwa hati kupitia mradi huo.

Ameeleza kuwa, Kamati yake ya PAC itakwenda kupima thamani ya fedha zilizopitishwa na Bunge pale tu wananchi watakapokuwa na hati.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amesema, wizara yake ina uhakika michakato yote itakapokamilika katika mji wa Nzega hati milki za ardhi zitaenda kutolewa kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Mhe, Pinda utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaenda kutoa jumla ya hati milki za ardhi 1,500,000 kwa maeneo yote yanayopotiwa na mradi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameweka wazi kuwa, kazi iliyofanyika kwa halmashauri ya Mji wa Nzega kwa sasa imefikia asilimia 55 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni asilimia 39.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unatekelezwa kwa mkopo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milionin150 kutoka Benki ya Dunia kwa kupindi cha miaka 5 katika halmashauri 58 nchini. Mradi huo unalenga kuboresha utawala na usimamizi wa ardhi nchini pamoja na kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa wananchi.