Back to top

“PSSSF ENDELEENI KULIPA MAFAO KWA WAKATI” SANGU

11 December 2025
Share

Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu imeupongeza Mfuko kwa kufikia thamani ya Tsh 12.55 trilioni kutoka Tsh 5.61 trilioni wakati mifuko minne inaungana mwaka 2018.

Mhe. Sangu alitoa pongezi hizo alipofanya ziara ya kikazi ya na kupokea taarifa ya utendaji wa PSSSF tangu kuteuliwa kwake kuongoza wizara hiyo inayosimamia Kinga ya Jamii ikiwemo PSSSF.

 “Napongeza kukua kwa thamani ya Mfuko iliyofikia ya trilioni 13 kutoka trilioni tano wakati mifuko ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF inaungana na kuunda PSSSF mwaka 2018 … hakika hatua hii ni kubwa mno na inatoa matumaini kwa wanachama wenu,” alisema Mhe. Waziri.

Mhe. Waziri aliitaka PSSSF kuendelea kulipa mafao kwa wakati na kuongeza, “Kabla ya kujiunga wizara hii, nilikuwa Wizara wa Utumishi ninajua jinsi PSSSF mnavyolipa mafao kwa wakati. Hongereni sana na endeleeni kuwalipa wastaafu mafao yao kwa wakati,” alisisita Mhe. Sangu.

Pia aliipongeza PSSSF kwa kufanikiwa katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha muda mfupi tangu kuazishwa, ikiwemo kuwahudumia wanachama wenu kidijitali kupitia huduma ya PSSSF Kidijitali.

Katika kuhakikisha Mfuko unakuwa imara, Mhe. Waziri aliitaka PSSSF kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kuhakikisha mipango yote ya PSSSF inazingatia mipango na dira ya taifa.

Akizungumzia utendaji kazi wa PSSSF, Mhe. Waziri alisema, “Nawapongeza PSSSF kwa kufanikiwa kuwanganisha pamoja watumishi waliotoka katika mifuko iliyounganishwa, nashauri mpango huo uendelee ili wafanyakazi wawe na utamanduni unaofanana katika kutoa huduma”.

Mhe. Sangu aliitaka PSSSF kuwekeza katika TEHAMA ili iweze kutrahisisjha katika utoaji huduma kwa wanachama wa Mfuko.

Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri alifuatana na Mhe. Rahma Riadh Kisuo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano na Bw. Festo Fute, Mkurugenzi wa Kinga ya Jamii katika Wizara ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu

Kwa upande wake, Mhe. Rahma Riadh Kisuo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano aliishauri PSSSF kuendelea kutoa elimu juu ya huduma zake ili wanachama wazijue vyema, kwani lengo la serikali inataka kila mstaafu apate haki yake kwa wakati na usahihi.

Kwa upande wake Murugenzi wa Mipango na Uwekezaji na Miradi wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo alimshukuru Mhe. Waziri Sangu kwa kukutana na Menejimenti na watumishi wa PSSSF.

“PSSSF tunaahidi kuendelea kutimiza majukumu yetu kwa uadilifu huku tukizingatia miongozo yote ya Serikali, tutahakikisha tunaendelea kulipa wastaafu wetu kwa wakati sahihi,” alisema Bw. Magambo.

Wakati tunaandaa taarifa hii Bw. Magambo ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, kwa mujibu wa Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari alasiri ya leo.