Back to top

2022 NI MWAKA WA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO.

01 January 2022
Share

Rais wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amesema mwaka 2022 utakuwa ni mwaka wa kukabiliana na changamoto zinazopunguza uwezo wa wananchi katika kukabiliana na maisha ya kila siku kwa lengo la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati wa hotuba yake ya kufungua mwaka kwa taifa na kutaja baadhi ya mafanikio na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi kwa mwaka 2022.

Katika hotuba yake amesema mwaka 2021 Tanzania imekuwa na ukuaji chanya wa uchumi kati ya nchi 54 za Afrika baada ya kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kiuchumi badala ya kuchukua hatua za kuwafungia kama ilivyokuwa nchi nyingine duniani.

Aidha Rais Mhe.Samia amesema hatua hiyo imekwenda sawia na kudhibiti mfumuko wa bei ambapo umeendelea kuwa asilimia 3 hadi tano na kuhakikisha nchi inak uwa na fedha za kutosha za kigeni ambazo zina uwezo wa kuagiza chakula kwa kipindi cha miezi saba.

Mbali na kuwatakia Watanzania wote heri ya mwaka mpya wa 2022 ameendelea kuwahimiza wananchi kuendelea kujitokeza katika vituo vinavyotoa huduma ya chanjo ya ugonjwa wa uviko 19 kufanya maamuzi ya kuchanja kwa lengo la kupunguza makali ya ugonjwa wa Corona mtu anapopata ugonjwa huo.