Back to top

Ajali ya boti yaua 30 katika ziwa Mai-Ndombe Congo DRC.

27 May 2019
Share

Watu 30 wamefariki na wengine zaidi ya 300 hawajulikani walipo baada ya boti kuzama katika ziwa Mai-Ndombe,Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Meya wa mji wa Inongo Simon Wemba, amelieleza shirika la habari la AFP kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba abiria zaidi ya 350, na watu waliookolewa ni 182 pekee.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Jumamosi katika ziwa Mai-Ndombe na Meya Wemba amesema imekuwa vigumu kuhesabu idadi kamili ya abiria kwa sababu wengi wanahofiwa kuwa wahamiaji haramu.

Boti hiyo pia inaaminika kuwa ilipakiza idadi kubwa ya walimu ambao walikuwa wanaelekea kupokea mishahara yao maeneo ya mijini.

Usafiri wa mito na maziwa ni moja ya usafiri unaotumiwa zaidi nchini jamhuri ya kidemokrasia ya  Congo DRC.

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni mwezi mmoja tu toka watu 167 walipofariki katika ajali mbili za majini ajali ambazo zilimlazimu rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo DRC bwana Felix Tshisekedi kuamrisha abiria wote wa vyombo vya majini nchini humo wavalishwe maboya muda wote wa safari.